Ikiwa imetimia siku ya nne tangu kuanza kwa zoezi la kukabidhi nyumba kwa wakazi 644 wa Magomeni Kota linaloratibiwa na Wakala wa Majengo Tanzania (TBA), idadi kubwa ya wakaazi wameendelea kujitokeza kwa ajili ya kukamilisha taratibu mbalimbali ili kukabidhiwa nyumba hizo, jambo linatoa taswira nzuri kuwa zoezi
linakwenda vizuri.
Akizungumza kwa niaba ya Wakala wa Majengo Tanzania TBA, Kaimu Meneja Mawasiliano kwa Umma na Masoko Bw. Fredrick Kalinga ameendelea kutoa taarifa juu ya zoezi hilo kuwa linakwenda vizuri na mpaka kufikia Machi 31, 2022 jumla ya kaya 306 kati ya kaya 644 zilikuwa zimeshapangiwa nyumba zao. "Leo Aprili 1 zoezi linaendelea na wakaazi wanaendelea kuonesha mwitikio mzuri hivyo tunategemea zoezi litakamilika ndani ya muda uliopangwa" aliongeza Bw. Kalinga
Wakiongea kwa nyakati tofauti wakaazi hawa wameonesha imani kubwa juu ya zoezi zima la ugawaji wa nyumba hizo kama asemavyo Bw. Majid Salum Mteleke “Hakuna matatizo yoyote, hitilafu ndogo ndogo ni vitu vya kawaida ukweli unabaki palepale kwamba kazi iliyofanyika ni nzuri sana”.
Aidha Bibi Sinahila Ramadhani hakuweza kuficha furaha yake baada ya kuiona nyumba yake na kusema “Nyumba ni ya kisasa sana,vitu vyote humu ndani ni vya kisasa yaani ujenzi huu umezingatia usasa wa ujenzi wa kipindi hiki tunashukuru sana sana Serikali ya Mama Samia Suluhu Hassan pamoja na Wakala wa Majengo (TBA) kwa nyumba hizi nzuri”. Wakiendelea kuonesha nia ya dhati ya kutunza makazi hayo, Bw. Majid Salum Mtekele aliongeza kwa kusema “hivyo walivyotutengenezea basi na sisi tuishi kwa hali tunayoiona tusiende tofauti.”
Zoezi la kuwapangia nyumba Wakaazi 644 wa Magomeni Kota linatarajia kuchukua takribani siku kumi tangu kuanza kwake 29 Machi, 2022.