WAKALA wa Majengo Tanzania (TBA) unajivunia kuwapa nafasi wanafunzi kutoka vyuo mbalimbali nchini kufanya mazoezi kwa Vitendo (Field attachment) katika miradi yake inayotekeleza mkoani Dodoma. Baadhi ya miradi mikubwa ya kimkakati ambayo TBA inatekeleza mkoani humo, ni ujenzi wa Mji wa Serikali, ujenzi wa nyumba 3500 za watumishi wa umma katika eneo la Nzuguni B, ujenzi wa nyuma za viongozi sambamba na ujenzi wa ofisi zingine za Serikali katika maeneo mbalimbali Dodoma.
Afisa Rasilimali watu ofisi ya TBA mkoa wa Dodoma, Bi Nashira Iddi anasema, tokea mwezi Januari hadi Septemba 2022, jumla ya wanafunzi 50 wamepokelewa na kufanya mafunzo kwa vitendo katika miradi hiyo.
“TBA tumeendelea kupokea wanafunzi kutoka vyuo mbalimbali kuja kujifunza kwa vitendo kwenye miradi yetu hapa Dodoma, tunaamini kuwa mafunzo hayo yatawasaidia katika taaluma zao.” Anabainisha Nashira
Patricia Olomi, ambaye ni mwanafunzi wa chuo kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), anayesomea Uhandisi ujenzi anasema, mafunzo hayo kwa vitendo yanawasaidia yanawaongezea maarifa na ujuzi katika fani zao.
Naye Brian Mushi, mwanafunzi wa chuo kikuu cha Ardhi, ambaye anasomea upimaji ardhi, amebainisha kuwa tangu wahudhurie mafunzo hayo, TBA inawapa ushirikiano mkubwa katika kutekeleza mafunzo hayo. “Wataalamu wa TBA wamekuwa msaada mkubwa sana kwetu, wanatufundisha kazi, hali hii inatuongezea ujuzi katika fani zetu”
Pamoja na uhandisi, pia wanafunzi wa kozi zingine ambazo ni uhasibu, manunuzi, ukadiriaji majenzi, ubunifu majengo, sheria na uendelezaji miliki wamepokelewa. Mbali na Chuo kikuu cha Dar es saalam na chuo cha Ardhi, wanafunzi wengine wanatoka vyuo vya CBE, SAUT-MZA, IFM, DIT, Chuo kikuu cha Sayansi na Teknolojia Mbeya (MUSTI) na VETA Dodoma.