Machi 15, 2024 Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu imetembelea na kukagua maendeleo ya mradi wa ujenzi wa nyumba za makazi katika eneo la Ghana Kota jijini Mwanza.
Akizungumza wakati wa ziara hiyo Mwenyekiti wa Kamati Mhe. Seleman Kakoso (Mb) ameagiza Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) kuwa na mkakati wa kujenga nyumba na kuziuza.“Muwe wabunifu kwa kuwa na mikakati ya kuwa na miradi ya kujenga nyumba za kuuza ili kujiongezea mapato na kupunguza utegemezi Serikalini” amesema Kakoso.
Pia Mhe. Kakoso ameiomba Serikali kuwapa TBA fedha ya kutosha kuendeleza maeneo mbalimbali inayomiliki. “Kwenye bajeti ijayo wafikirieni TBA, wawezesheni bilioni hamsini (50) tuu. Wakiwa na bilioni hamsini watajenga majengo kule Arusha, wana maeneo mazuri sana Arusha, watajenga Dar es Salaam pale Magomeni Kota wana eneo kubwa sana liko wazi na lina uwezo wa uwekezaji mkubwa sana, Mheahimiwa Waziri hawa TBA wanaweza wakakufanya ukapata mapinduzi makubwa sana wakakuona Waziri umekuja na vision ya ajabu kwa fedha ndogo tuu mtakazowekeza hapa” amesema Kakoso.
Aidha Mhe. Kakoso ameitaka TBA kuhakikisha kuwa maeneo yote yenye migogoro yanawekewa mikakati ya kuyamiliki kisheria na kuwa na mpango wa kuyaendeleza kwa kubuni majengo yenye mvuto ili kupata wateja.
Awali akitoa taarifa ya utekelezaji wa mradi Mtendaji Mkuu wa TBA Arch. Daud Kondoro alisema kuwa mradi umefikia asilimia 50 za utekelezaji ambapo fedha takribani bilioni 2.1 za vyazo vya ndani zimetumika. Pia Arch. Kondoro alisema kuwa mradi huo unatekelezwa kwa kuzingatia taratibu za mipango miji, sheria na miongozo yote ya ujenzi pamoja na kuzingatia viwango vya ubora.
Mradi wa ujenzi wa nyumba za watumishi wa umma awamu ya kwanza katika eneo la Ghana Kota jijini Mwanza unajumuisha ujenzi wa jengo la ghorofa lenye sakafu saba pamoja na majengo mawili ya maduka yenye sakafu mbili ambayo yatakuwa na jumla ya maduka 39 kwa ajili ya kutoa huduma mbalimbali za kijamii kwa watakaokuwa wakaazi wa nyumba zinazojengwa na wananchi wanaoishi karibu na eneo hilo.