Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu ikiongozwa na Mwenyekiti wake Mhe. Selemani Kakoso (Mb) imefanya ziara ya kutembelea na kukagua maendeleo ya utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa nyumba za makazi ya watumishi wa umma katika eneo la Temeke Kota jijini Dar es Salaam.
Akizungumza katika ziara hiyo Mhe. Kakoso amesema TBA imekuwa ikifanya kazi kubwa katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ya ujenzi wa nyumba za makazi hususani mradi wa ujenzi wa Temeke Kota. Amesema kuwa ni vyema Wizara ikasaidia upatikanaji wa fedha kwa wakati ili mradi huo uweze kutekelezwa kwa wakati uliokusudiwa.
Aidha, Mhe. Kakoso amesema ni wakati sahihi sasa TBA kuanza kujiendesha kibiashara kwa kushirikiana na Sekta Binafsi na kuacha kutegemea fedha za ruzuku kutoka Serikalini kutekeleza miradi yake.
Pia Mhe. Kakoso ameitaka Wizara ya ujenzi kuisaidia TBA kudai madeni kutoka taasisi mbalimbali za Serikali. "TBA inapitia kipindi kigumu kwasababu ya kuwa na malimbikizo makubwa ya madeni kutoka taasisi mbalimbali hivyo ni vyema Wizara ya Ujenzi mkaisaidia ili fedha hizo ziende kufanya uwekezaji mkubwa zaidi" amesema Mhe. Kakoso.
Naye, Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Mhe. Prof. Makame Mbarawa (Mb) amesema amepokea maelekezo yote yaliyotolewa na Kamati ya Miundombinu na kuahidi kwenda kuyafanyia kazi. Pia Mhe. Mbarawa ameipongeza TBA kwa hatua inazochukua kuwaondoa wadaiwa sugu na kuwaelekeza wapangaji wa nyumba za TBA kulipa kodi ya pango kwa wakati vinginevyo wataondolewa katika nyumba hizo kama ambavyo zoezi la kuwaondoa linavyoendelea.
Kwa upande wake Mtendaji Mkuu wa TBA Arch. Daud Kondoro ameishukuru Kamati kwa kufanya ziara hiyo na kuahidi kuyafanyia kazi maelekezo na mapendekezo yote yaliyotolewa.
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu imefanya ziara ya katika mradi wa Ujenzi wa nyumba za watumishi wa Umma unaotekelezwa na TBA kama Mkandarasi na Mshauri Elekezi katika eneo la Temeke Kota.