Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan, amepongeza na kuridhishwa na ujenzi wa Kituo cha pamoja cha forodha katika mpaka wa Tanzania na Malawi kilichojengwa katika eneo la Kasumulu Wilayani Kyela mkoani Mbeya na kueleza kuwa Kituo hicho kitasaidia kukuza uchumi kwa wananchi na Taifa kwa ujumla. Amesema hayo Agosti 7, 2022 baada ya kuweka jiwe la msingi katika Kituo hicho.
Aidha Rais Samia amebainisha kuwa Kituo hicho ni muhimu kwa kuwa kitawezesha wananchi kufanya biashara kwa urahisi na kujiletea maendeleo.
Awali akitoa maelezo kwa Mhe. Rais Samia, Mtendaji Mkuu wa TBA, Arch. Daudi Kondoro amesema ujenzi huo unajumuisha eneo la maegesho ya magari ambalo lina uwezo wa kuchukua Mabasi 18, magari madogo 22. Pia kuna eneo la magesho ya malori.
Amefafanua kuwa mradi huo pia unahusisha jengo la abiria lenye sehemu za kukagua mazao na bidhaa nyingine. Pia kuna sehemu za usalama kwa ajili ya kupima afya za abiria na endapo itabainika kuna mgonjwa, ipo sehemu ya Karantini ya kumhifadhi mgonjwa huyo kwa muda.
Wananchi waliohudhuria hafla hiyo, wameshukuru na kupongeza ujenzi huo kuwa utachochea maendeleo katika kwa kiasi kikubwa.
Mradi huo unajengwa na Kampuni ya China Geo-Engineering Corporation (CGC) na kusimamiwa na Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) kwa kushirikiana na Kampuni ya Engineering Consultant Group (ECG) kutoka Misri.