Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango ameupongeza kwa Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) kwa kufanikisha kukamilisha ujenzi wa jengo la kisasa la makazi kwa kuzingatia ubora, tija, gharama nafuu pamoja na kuwa na huduma kisasa zinazoendana na mahitaji ya teknolojia.
Makamu wa Rais amesema hayo leo tarehe 04 Agosti 2023 wakati wa Hafla ya Ufunguzi wa Jengo la makazi la Kibiashara lililopo eneo la Sekei jijini Arusha ambalo limejengwa na Wakala wa Majengo Tanzania (TBA)
Ameongeza kwamba ni vyema TBA ikafanya mapinduzi makubwa ya kiutendaji, kuongeza ubunifu na kujenga misingi mizuri ya kujiendesha kibiashara ili kuweza kupata mapato zaidi na kujiendesha pasipo kutegemea ruzuku kutoka serikalini.
Halikadhalika Makamu wa Rais amewataka TBA kuweka utaratibu shirikishi kwa lengo la kuimarisha ulinzi na usalama wa watu na mali zao katika maeneo ya nyumba hizo. Pia amewasihi wapangaji watakaopanga kwenye nyumba hizo kuzitunza na kuhakikisha zinabaki katika hali ya ubora wake ikiwemo kuzingatia masuala ya usafi na utunzaji wa mazingira.
Makamu wa Rais amesema uwekezaji katika Sekta ya ujenzi ni miongoni mwa vipaumbele muhimu vya Serikali ya Awamu ya Sita ambayo inaendelea kuhakikisha miradi hiyo inatekelezwa kama ilivyopangwa. Aidha amesema Serikali itaendelea kuunga mkono ubunifu na mipango ya Taasisi kama TBA kuwa na miradi mingi zaidi ya ujenzi ili kuongeza makusanyo ya ndani na kupunguza utegemezi wa ruzuku kutoka Serikalini.
Naye Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Profesa Makame Mbarawa amesema kukamilika kwa jengo hilo kutasaidia upatikanaji wa makazi ya uhakika kwa wakaazi waliopo jijini Arusha.
Profesa Mbarawa ameongeza kwamba ujenzi wa mradi huo umesaidia Wataalamu wazawa wa fani za ujenzi kujengewa uwezo wa taaluma kwa vitendo pamoja na kusaidia kuendelea kukua kwa kasi kwa jiji la Arusha lililopangwa vizuri kwa kuzingatia mipango miji, kuongezeka kwa mapato ya serikali na huduma za kijamii katika jiji hilo.
Awali akitoa taarifa ya utekelezaji wa mradi huo, Mtendaji Mkuu wa TBA Arch. Daud Kondoro amesema jengo hilo la makazi lina sakafu 12 ikijumuisha sakafu moja iliyo chini ya usawa wa ardhi (basement) itakayotumika kama sehemu ya kuhifadhia (storage). Katika sakafu 11 zilizobaki, kila sakafu ina nyumba (apartments) mbili (2) na hivyo kulifanya jengo hili kuwa na uwezo wa kuchukua jumla ya familia 22.
Kandoro amesema TBA inaendelea kutekeleza miradi mingine nchi nzima kwa fedha za ruzuku na makusanyo ya ndani ikiwemo mradi wa ujenzi wa nyumba mpya 20 za Viongozi katika eneo la Kisasa Dodoma, ukamilishaji wa nyumba za majaji kwenye Mikoa ya Kilimanjaro, Mtwara, Shinyanga, Tabora na Kagera, ukarabati wa nyumba za makazi ya watumishi wa Umma na Viongozi Tanzania Bara ili kuwawezesha kuishi katika mazingira bora, Ujenzi wa nyumba za makazi kwa Watumishi wa Umma katika eneo la Magomeni Kota na Temeke Kota, Ujenzi wa jengo la makazi eneo la Masaki,pamoja na ujenzi wa nyumba 13 za watumishi Mikoani.