Wanawake
wa Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) walipata fursa ya kushiriki maadhimisho ya
siku ya wanawake duniani Machi 8, 2020 katika maeneo mbalimbali nchini yenye
kauli mbiu “Kizazi cha Usawa kwa Maendeleo ya Tanzania ya sasa na baadaye”. Pia
walipata nafasi ya kutembelea Hospitali ya Amana jijini Dar es Salaam na
kutembelea Kituo cha watoto yatima cha TCRC kilichopo Nyansaka jijini Mwanza.
Katika
Mkoa wa Dar es Salaam kongamano la maadhimisho ya siku ya wanawake lilifanyika katika
viwanja vya Leaders, Kinondoni ambapo Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Mhe. Paul Makonda
alikuwa mgeni rasmi. Katika hotuba yake, Mkuu wa Mkoa alisema hataki kumwona
mwanamke yeyote katika mkoa anaouongoza akinyanyasika, ndio maana aliamua
kuwasaidia wanawake waliotelekezwa na wenza wao na kutoa namba za mawasiliano
ambayo wanaweza kupiga bure.
Aidha,
katika Mkoa wa Mwanza wanawake wa TBA walishiriki maadhimisho siku ya wanawake duniani
katika viwanja vya Furahisha ambapo Mgeni rasmi alikuwa Mkuu wa Wilaya ya
Nyamagama Mhe. Dkt. Philis M. Nyimbi ambaye alisisitiza umuhimu wa wanawake
kupewa mikopo, kupewa kipaumbele katika nyanja mbalimbali pamoja na kuthubutu
kushiriki katika vinyang’anyiro vya kugombea nafasi mbalimbali za Uongozi bila
kusubiri upendeleo wa viti maalum.
Katika
kuadhimisha siku ya wanawake duniani, wanawake wa TBA walipata nafasi ya
kutembelea Hospitali ya Amana jijini Dar es Salaam na kutoa vifaa tiba pamoja
na mashuka kwa mama wajawazito. Vile vile Mkoani Mwanza wanawake wa TBA
walitembelea kituo cha watoto yatima cha TCRC kilichopo Nyansaka na kutoa mahitaji
mbalimbali yakiwemo mahindi gunia 3, sukari kilo 25, sabuni ya unga, mchele
kilo 100, taulo za kike pamoja na mahitaji mengine ya msingi.