“Kizazi cha haki na usawa kwa maendeleo endelevu” ni kauli mbiu iliyobeba maadhimisho ya siku ya wanawake duniani yaliyofikia kilele chake mnamo Machi 8, 2022. Maadhimisho hayo yaliambatana na maandamano yaliyofanyika katika mikoa mbalimbali nchini pamoja na maonyesho ya bidhaa mbalimbali zilizotengenezwa na wanawake wajasiriamali.
Wafanyakazi wanawake wa Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) waliungana na wanawake wengine dunia kusherehekea maadhimisho hayo ambayo yalifanyika katika mikoa mbalimbali nchini.
Viongozi mbalimbali walioudhuria sherehe hizo waliwapongeza wanawake na kuwataka waendelee kufanya kazi kwa bidii. Akizungumza wakati wa sherehe hizo Bw. Hassan Rugwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Dar es Salaam alitoa ujumbe kwa wanawake wa Dar es Salaam kuwa Serikali inaendelea kuongeza kiwango cha mikopo kwa wanawake.
Awali Mtendaji Mkuu wa TBA Arch. Daud Kondoro alitoa baraka zake kwa wanawake wa TBA kabla ya kuanza kwa maandamo hayo katika Makao Makuu ya ofisi za Wakala jijini Dar es Salaam. Pia Arch. Kondoro aliwapongeza wanawake wa TBA kwa kazi nzuri wanazozifanya kila mmoja katika kitengo chake ambazo zimekuwa chachu ya mafanikio ya Wakala na taifa kwa ujumla. "Kama kauli mbiu yenu inavyosema Kizazi cha haki na usawa kwa maendeleo endelevu hivyo kila mnachokipata hapa TBA ni haki yenu" aliongeza Arch. Kondoro.
Wanawake wa TBA wamemshukuru Mtendaji Mkuu pamoja na menejimenti ya TBA kwa kuwawezesha katika maeneo mbalimbali.