WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa Januari 16, 2022 amekagua maendeleo ya ujenzi wa Ikulu inayojengwa katika eneo la Chamwino, Jijini Dodoma na kusema ameridhishwa na kasi ya ujenzi na ubora wa majengo hayo na amemtaka mkandarasi ahakikishe mradi huo unakamilika mwezi mei mwaka huu.
Waziri Mkuu amewasisitiza wakandarasi kuhakikisha wanakamilisha mradi huo kwa wakati na kuwapongeza wote wanaohusika na ujenzi wa mradi huo “
“Nimefurahishwa na taarifa kwamba ujenzi huu umefikia asilimia 91 na hatua iliyobaki hizi asilimia 9 ni kazi ndogondogo kama uwekaji wa milango, njia za mifumo ya hewa na umeme na zote zinaenda vizuri.” Waziri Mkuu amesema kuwa Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan pia anatarajia kuona ujenzi huo unakamilika kwa wakati.
Kwa Upande wake Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Majengo Tanzania (TBA), Arch. Daudi Kondoro amemhakikishia Mheshimiwa Waziri Mkuu kwamba mradi huo utakamilika na kukabidhiwa mwezi Mei kama inavyotarajiwa kwani sasa uko katika hatua za mwisho za ukamilishaji.
Mradi wa Ujenzi wa Ikulu ya Chamwino unatekelezwa na TBA kama Mshauri Elekezi pamoja Suma JKT kama Mkandarasi.