Bodi ya Ushauri ya TBA imefanya kikao chake cha pili cha kawaida kwa mwaka wa fedha 2023/24 katika ukumbi wa mikutano wa TBA uliopojijini Dar es Salaam.
Akizungumza baada ya kumalizika kwa kikao hicho Mwenyekiti wa Bodi hiyo Arch. Ombeni Swai amesema miongoni mwa masuala yaliyojadiliwa ni pamoja na mapendekezo ya bajeti ya Wakala kwa mwaka 2024/25.
“Kupitia Bajeti hiyo ya Wakala, Bodi imeichambua na kuja na mapendekezo mbalimbali ambayo yanalenga kuiwezesha TBA kufanya kazi kwa ufanisi. Vile vile Bodi imebaini kazi kubwa iliyofanywa na TBA katika makusanyo ya kodi kutoka katika nyumba na majengo yanayosimamiwa na TBA nchini” amesema Arch. Swai.
Aidha amesema kupitia kikao hiki Bodi imetoa maelekezo kwa Menejimenti ya TBA kuhakikisha wanaongeza kasi ya ukusanyaji wa kodi ya pango sambamba na kuwaondoa wadaiwa sugu ili kuhakikisha mapato yanayokusanywa yanakwenda kutekeleza majukumu mengine ikiwa ni pamoja na ujenzi wa nyumba mpya na ukarabati.
Katika hatua nyingine Arch. Swai ameipongeza TBA kwa kuendelea kutekeleza miradi mbalimbali kwa weledi na ufanisi.
“Baada ya kupitia taarifa mbalimbali zilizowasilishwa na Menejimenti ya TBA, nawapongeza kwa kazi nzuri wanayoendelea kuifanya hasa katika ujenzi wa nyumba mpya katika maeneo mbalimbali nchini” amesisitiza Arch. Swai.