Wakala wa Majengo Tanzania
(TBA), umepata Mtendaji Mkuu mpya Arch. Daud W. Kondoro ambaye ameidhinishwa
rasmi kuiongoza Taasisi hii akichukua nafasi ya aliyekuwa Mtendaji wake Mkuu,
Arch. Elius A. Mwakalinga ambaye aliteuliwa kuwa Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi,
Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Ujenzi).
Kabla ya kuidhinishwa rasmi,
Arch. Kondoro alikuwa anakaimu nafasi hiyo kwa kipindi chote ambacho Arch.
Mwakalinga ameteuliwa kuwa Katibu Mkuu.
Akiwasilisha taarifa za
udhibitisho/uteuzi huo kutoka kwa Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
Mhandisi Isaack Kamwelwe, Katibu Mkuu Mwakalinga amesema Waziri ameridhika na
utendaji kazi wa TBA hivyo amemthibitisha rasmi Arch. Daud W. Kondoro kuwa
Mtendaji Mkuu wa TBA.
Aidha, Katibu Mkuu
Mwakalinga, ameishukuru TBA kwa kazi inayoendelea kufanya kwa kuzingatia
viwango vya ubora, gharama nafuu na muda wa utekelezaji. Alipongeza kazi
inayofanyika katika miradi mbalimbali mikoani huku akitaja baadhi ya miradi mikubwa
kama vile nyumba za makazi Magomeni Kota na Mji wa Serikali Chamwino.
Naye Mtendaji Mkuu mpya Arch.
Kondoro, ameshukuru Mamlaka ya Uteuzi kwa kuwa na imani naye na kuahidi
kutekeleza majukumu aliyopewa kwa weledi na kwa uwezo wake wote. Pia ameishukuru
menejimenti na wafanyakazi wote wa TBA kwa ushirikiano waliompa kwa kipindi
chote alichokuwa anakaimu nafasi hiyo, na kuomba ushirikiano huo uendelee ili
kutekeleza malengo ya Taasisi kwa weledi na mafanikio zaidi.
Arch. Daud W. Kondoro anakuwa
Mtendaji Mkuu wa tatu kushika wadhifa huo tangu TBA ilipoanzishwa mwaka 2002.