Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) utaendelea kuwa Wakala bora kwa kutumia wataalam iliyonao kutekeleza miradi ya Serikali kwa weledi na kuzingatia ubora.
“Siri kubwa ya kukamilika kwa Miradi
ni kutokana na kupata fedha kwa wakati”
Mtendaji
Mkuu wa TBA, Arch. Daudi Kondoro amebainisha hayo akijibu swali la Mwandishi wa
Gazeti la Serikali la Daily News katika mahojiano maalumu yaliyofanyika Jijini Dodoma
hivi karibuni.
“Sisi kama TBA kwa kawaida hatuwezi
kwenda hatua nyingine ya ujenzi bila ya kujiridhisha hatua tuliyomaliza kama ipo
sahihi, hasa kwa kuangalia mahitaji yaliyohitajika katika hatua hiyo” amesisitiza Arch. Kondoro
Arch.
Kondoro, ameitaja miradi ya Wilaya ya Kigamboni ambayo ni ujenzi wa Ofisi za
Mkuu wa Wilaya na Mkurugenzi wa Manispaa zilizokamilika hivi karibuni na
kukabidhiwa kwa wakati, kuwa ni
kielelezo tosha cha ubora, weledi na gharama nafuu, hali inayochangiwa na
upatikanaji wa fedha kwa wakati.
Ameeleza
kuwa baadhi ya miradi mikubwa ya Kitaifa ambayo TBA inasimamia ni pamoja na
ujenzi wa Rada katika Kiwanja cha ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere
(JNIA), Kiwanja cha ndege cha Kimataifa cha Kilimanjaro (KIA), Kiwanja cha
ndege cha Kimataifa cha Songwe na kiwanja cha ndege cha Mwanza, ujenzi wa Kituo
cha pamoja cha forodha kinachojengwa katika mpaka wa Tanzania na Malawi eneo la Kasumulu , Mkoani Mbeya na mradi wa
ujenzi wa Maghala ya kuhifadhi chakula maarufu kama Vihenge ambao unatekelezwa
katika mikoa nane ya Dodoma, Katavi, Ruvuma, Njombe, Songwe, Rukwa, Shinyanga na
Manyara.
“Mradi wa ujenzi wa maghala ya
kuhifadhia chakula, umefikia asilimia 80 kukamilika, mradi huu ni wa Kitaifa
ambao unatekelezwa katika mikoa 8. Tuna matumaini mradi huu ukikamilika utakuwa
ni msaada mkubwa katika uhifadhi wa chakula nchini”
Kwa
upande wa vifaa, Mtendaji Mkuu amefafanua kuwa TBA ina mitambo miwili (2) ya
kuchakata zege, mmoja umefungwa Dar es Saalam katika mradi wa Magomeni Kota na
mwingine upo Nzuguni mkoani Dodoma. Pia TBA ina kiwanda cha kutengeneza tofali
ambacho kipo Magomeni. Ametaja faida ya kiwanda hicho kuwa kinauwezo wa kutengeneza
tofali zaidi ya 2000 kwa siku, na matofali hayo yanatumika katika ujenzi wa
nyumba za Magomeni Kota, hivyo kimesaidia kupunguza gharama.
Naye
Mkurugenzi wa Ushauri Arch. Wenceslaus Kizaba akizungumzia ujenzi wa Mji wa
Serikali amesema, michoro ya majengo kwa awamu ya pili imekamilika na
kupitishwa na Mamlaka husika tayari kwa utekelezaji unaofuata ambao ni ujenzi.
Ujenzi
wa mji wa Serikali awamu ya pili utabadilisha muonekano wa mandhari yaliyopo
kwa sasa, kwa kuwa na majengo ya ghorofa, barabara za lami na mazingira yenye
kuvutia.
Wakala
wa Majengo Tanzania (TBA) ni taasisi ya Serikali iliyoanzishwa mwaka 2002 kwa
lengo la kusimamia miliki za Serikali.