Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni Mhe. Daniel Chongolo atembelea mradi wa ujenzi wa nyumba za makazi ya wananchi Magomeni kota uliosanifiwa na kujengwa na Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) na kuridhishwa na kasi ya ujenzi wa mradi huo unaotarajiwa kukamilika mnamo mwezi Desemba mwaka huu.
Katika ziara yake Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni
alitembelea majengo ya magorofa yanayojengwa, kiwanda kidogo cha kufyatua
tofali pamoja na mtambo wa kuchakata zege (Batching Plant) na kujionea namna
ambavyo TBA unatumia kikosi chake maalum cha ujenzi (TBA Brigade) katika
kupunguza gharama za ujenzi. Vile vile uwepo wa viwanda hivi vidogo unapunguza
gharama za mradi kwa kuwa malighafi nyingi za ujenzi zinazalishwa na TBA na
kuepuka kununua kutoka kwa wazabuni ambao bei zao zipo juu.
Akizungumza wakati wa ziara, Mkuu wa Wilaya
ya Kinondoni amesema “Napenda kuchukua fursa hii kuwapongeza TBA kwa kuwa
wazalendo na kuamua kutumia kikosi kazi chake cha ujenzi katika kuandaa tofali
na kuchakata zege ili kupunguza gharama za mradi na pia kwa kuwatumia vijana wa
maeneo jirani na mradi kama vibarua na mama lishe katika kutoa huduma kwenye
eneo la mradi kwani hiyo imetoa fursa kwa wakazi wa wilaya ya Kinondoni
kujipatia kipato”
Akiuelezea mradi huo Meneja wa mradi kutoka TBA Mbunifu Majengo Bernard Mayemba amesema “Mradi huo unatarajiwa kukamilika ifikapo mwezi Desemba mwaka huu endapo hapatatokea changamoto zozote za kiutendaji”. Mradi huu unategemewa kuchukua jumla ya kaya 656 ikiwa ni utekelezaji wa agizo la Mhe. Rais Dkt. John Pombe Magufuli la kujenga kaya 644. TBA inachukua jitihada za haraka kuukamilisha mradi huu kwa kufanya kazi usiku na mchana ili kufikia malengo hayo.