Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Ujenzi) Arch. Elius Mwakalinga leo Oktoba 20, 2020 ametembelea na kukagua maendeleo ya mradi wa Ujenzi wa nyumba za makazi ya wananchi Magomeni Kota jijini Dar es Salaam. Mradi huo unatarajiwa kutoa makazi kwa kaya takribani 656 ambazo zitaishi katika eneo hilo.
Baada ya kutembelea mradi huo Katibu Mkuu amewapongeza na kuwashukuru Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) ambao ni wakandarasi na wasimamizi wa mradi huo kwa hatua nzuri ya maendeleo ambayo mradi huo umefikia. Hata hivyo, Katibu Mkuu amesema Serikali kupitia Wizara ya Ujenzi imewapatia TBA kiasi cha shilingi bilioni 9 ili ziweze kusaidia kukamilika kwa mradi huo unaotarajiwa kukamilika Januari 2021.
Aidha, Arch. Elius Mwakalinga amesema mradi huo utakuwa na miundombinu wezeshi kwa wakazi wa eneo hilo Kutokana na uwepo wa huduma mbalimbali za kijamii katika eneo la mradi kama vile Masoko, Maduka, Maeneo ya kupumzika, Sehemu za kufulia pamoja na uwepo wa vifaa vya kujikinga na janga la moto. Akizungumza katika ziara hiyo Arch. Elius Mwakalinga ameipongeza serikali ya awamu ya tano kwa kuwajali wananchi wake na kuweza kufanikisha maendeleo ya Ujenzi wa mradi huo wa Magomeni Kota.
Vilevile, Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) Arch. Daud W. Kondoro amesema ujenzi huo mpaka sasa umekamilika kwa asilimia themanini na moja (81%) hivyo mpango mkakati wa TBA kwa sasa ni kufanya kazi usiku na mchana ili kukamilisha mradi huo ifikapo Januari 2021.
Pia, Mtendaji Mkuu amesema mradi huo haukuathiriwa na ugonjwa wa Corona kwa kuwa vifaa vingi vya Ujenzi vinanunuliwa ndani ya nchi.
Mradi wa nyumba za makazi Magomeni kota unatekelezwa ikiwa ni ahadi ya Rais wa awamu ya tano wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli.