Wabunge wameshauri Serikali kuendelea kuiwezesha TBA ili iweze kutekeleza mipango yake kwa ufanisi.
Wakizungumza Bungeni jijini Dodoma mara baada ya Waziri wa Ujenzi Mhe. Innocent Bashungwa kuwasilisha Bajeti ya Wizara hiyo, wamesema Serikali iendelee kuongeza fedha ili TBA iweze kujiendesha zaidi kibiashara na kuzalisha faida.
Akichangia hoja hiyo, Mbunge wa Viti maalam vijana Mhe. Amina Ali Mzee amesema TBA inajitahidi kuhakikisha kuwa wananchi na watumishi wa umma wanaishi katika makazi bora hivyo Serikali iunge mkono juhudi hizo kwa kuongeza fedha ili miradi iliyopangwa kutekelezwa ikamilike na kuanzisha miradi mingine.
"Nitoe wito kwa wananchi na Taasisi za Serikali zinazodaiwa na TBA ziweze kulipa madeni yao" amesisitiza Mhe. Amina.
Mbunge mwingine, Bi. Saada Hussein ambaye ni mbunge wa viti maalum Pemba amesema, TBA wanafanya kazi nzuri hivyo wanatakiwa kuwezeshwa zaidi ili kukamilisha miradi yake.
"Mhe. Spika wapo pia wabunge na wananchi wanaodaiwa na shirika hili la TBA, hivyo linashindwa kujiendesha vizuri, tunaomba wale wote wanaodaiwa waweze kulipa kodi ya pango hizo" anasema Mhe. Saada.
Naye mbunge wa Ilemela Dkt. Angeline Mabula ametoa rai kwa TBA kuendelea kuwekeza zaidi katika miradi ya ubia, akitolea mfano mkoa wa Mwanza ambao una fursa nyingi za uwekezaji zikiwemo kumbi za mikutano, hoteli na nyumba za makazi.
Hivi karibuni TBA, imefanya marekebisho ya sheria ya kuanzishwa kwake ambayo sasa inaruhusu TBA kuanza kutekeleza miradi ya ubia kwa kushirikiana na Sekta binafsi.