Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dk. Philip Isdor Mpango amezindua rasmi jengo la huduma ya afya ya mama na mtoto katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mwanza Sekou – Toure ambalo limebuniwa na kujengwa na Wakala wa Majengo Tanzania (TBA).
Akizingumza wakati wa hafla ya uzinduzi Mhe. Dkt. Mpango amesema ni vema kuhakikisha mama na mtoto anapata lishe bora kwa manufaa ya jamii na taifa kwa ujumla.
"Mtoto akipata lishe bora anaepuka magonjwa ya mara kwa mara na itasaidia kupunguza gharama ambazo zingetumika kwenye matibabu. Ni vema kuchukua hatua ili miaka ijayo kuwa na taifa lenye watu wenye uwezo wa kufikiri na kufanya kazi kwa tija. Upatikanaji wa huduma za afya kwa mama na mtoto bado ni changamoto licha ya jitihada za serikali kuhakikisha zinapatikana kwa watanzania wote", amesema Dkt. Mpango.
Hata hivyo, Mhe. Dkt. Mpango ameongeza kuwa serikali itaendelea kutenga fedha kwa ajili ya kuboresha miundombinu ya afya nchini kwa kusogeza huduma kwa wananchi hasa wa vijijini.
Vile vile Mhe. Dkt. Mpango ameupongeza Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) kwa kusimamia na kujenga jengo hilo na kupelekea kukamilika na kuanza kutumika.
Akizungumza wakati wa hafla hiyo Mtendaji Mkuu wa TBA Arch. Daud Kondoro amesema wameshiriki kwenye ujenzi huo kwa kutoa huduma ya Ushauri Elekezi na Ukandarasi.
"Tumeshiriki katika kubuni, kusanifu na kujenga mpaka kumalizika kwa jengo hili na tumefanya ubunifu kwa kupima udongo katika eneo hili ili jengo liwe na uimara wa kutoa huduma inayotakiwa," amesema Arch. Kondoro.
Amesema katika ujenzi na ubunifu wamezingatia mambo muhimu ili kuhakikisha huduma mbalimbali zinapatikana ikiwemo maji kwani kuna tanki la maji lenye lita za ujazo 150,000 linaloweza kutoa huduma muda wote.
Naye Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mwanza Sekou - Toure Dkt. Bahati Msaki amesema jengo hilo lilianza kujengwa mwaka 2017 na limegharimu fedha kiasi cha shilingi bilioni 12.9 hadi kukamilika kwa ujenzi huo.
"Jengo hili limeanza kutoa huduma mwezi Mei mwaka 2022 ambapo mradi huo umeboresha huduma ya afya kwa wananchi wakiwemo akina mama na watoto. Jengo hili litapunguza msongamano wa wagonjwa uliokuwepo awali ambapo kulikuwa na vitanda 140 na katika jengo jipya kuna vitanda 261. Uwepo wa jengo hili utasaidia kupunguza vifo vya wajawazito na watoto ambapo jengo hilo tangu lianze kutoa huduma limeshahudumia wanawake 1883 na watoto 800" amesema Dkt. Msaki.