Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi (Sekta ya Ujenzi) Mhe. Mhandisi Godfrey Kasekenya leo januari 10, 2023 amefanya ziara ya Kutembelea na kukagua maendeleo ya mradi wa ujenzi wa nyumba za makazi kwa ajili ya Watumishi wa Umma katika eneo la Magomeni Kota, jijini Dar es Salaam.
Akizungumza baada ya kukagua mradi huo Mhe. Kasekenya amesema utekelezaji wa mradi huo ni kwa ajili ya kutatua changamoto ya makazi.
" ujenzi huu ni kwa ajili ya kutatua changamoto ya makazi na ambapo kwa matarajio katika eneo hili kutajengwa majengo matato (5) ya ghorofa nane".
Pia Mhe. Kasekenya amepongeza ujenzi wa mradi huo.
" nimelitembelea jengo ni zuri na lina miundombinu ya kisasa, jengo hili litakuwa la ghorofa 8 ambapo kila ghorofa litachukua kaya mbili. Hivyo nipende kumshukuru Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kutoa fedha kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali" amesema Mhe. Kasekenya.
Aidha, Mhe. Kasekenya Ametoa wito kwa TBA kuendelea kuzingatia gharama za ujenzi ili kuendana na mahitaji husika.
Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu wa TBA Arch. Daud Kondoro ameahidi kufanyia kazi maelekezo yalitolewa na Mhe. Kasekenya.
" tumepokea maelekezo ya Mhe. Naibu Waziri na pia ikumbukwe kuwa gharama za matumizi ya ujenzi zimekuwa zikihakikiwa na Wizara ya Ujenzi na ni utaratibu wa kawaida ambao unafanyika siku zote."
Mradi wa ujenzi wa Nyumba za makazi kwa ajili ya Watumishi wa Umma awamu ya pili katika Eneo la Magomeni Kota umefikia Asilimia 96 ambapo TBA inatekeleza mradi huo kama Mkandarasi na Mshauri Elekezi.