Takribani Wahasibu hamsini na tisa (59) kutoka katika ofisi zote za Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) kote nchini wameshiriki kikao kazi kilichofanyika kwa muda wa siku tatu kuanzia Septemba 21- 23, 2022 katika ukumbi wa mikutano uliopo kwenye ofisi za Meneja wa TBA mkoa wa Dar es Salaam.
Akizungumza wakati wa kufunga kikao kazi hicho, Mtendaji Mkuu TBA Arch. Daud Kondoro amewapongeza washiriki wote kwa kushiriki ipasavyo katika kikao kazi hicho na kuwaasa wahasibu wote kusimamia matumizi mazuri ya fedha za serikali hali itakayosaidia kuipunguzia serikali hasara sambamba na kusimamia vyema miradi yote inayotekelezwa na Wakala kwa manufaa ya taifa kwa ujumla. Vile vile Mtendaji Mkuu amewataka wahasibu hao kuishauri vyema Menejimenti ya TBA na kuhakikisha kuwa wanashirikiana vyema ikiwa ni pamoja na kutoa mrejesho, jambo litakalosaidia kutambua ni kwa kiasi gani malengo waliyojiwekea yamefikiwa.
Akizungumza kwa niaba ya washiriki hao, Mwenyekiti wa kikao kazi hicho CPA Selemani Mbuse, amesema mafunzo waliyoyapata katika kikao kazi hicho, yatawasaidia kuandaa taarifa nzuri za fedha zenye viwango vya kimataifa na zinazokidhi vigezo vya kimataifa na kwamba mafunzo hayo yaendelee kwani yanasaidia kuwajengea uwezo na kuwakumbusha wahasibu sheria, kanuni, na miongozo ya ndani na kimataifa kwenye kufunga hesabu pamoja na kufanya kazi kwa kuzingatia maboresho ya mifumo mbalimbali ya fedha za serikali.