“Nawapongeza sana TBA kwa mapinduzi makubwa ambayo tunayaona juu yenu mmekuwa ni wabunifu lakini mmejua kubadilika kutokana na mahitaji, sasa hivi mmeaminiwa sana na serikali, mmepewa miradi mikubwa sana lakini hakuna mliokwama kila mradi unaenda kisasa”.
Ndivyo anavyoanza kueleza Mhe. Rosemary Senyamule, Mkuu wa Mkoa wa Geita baada ya kutembelea Banda la TBA. Akionekana mwenye uso wa tabasamu uliojaa furaha, anavutiwa na mapinduzi yanayofanywa na TBA kila uchao upande wa ubunifu wa majengo na jinsi inavyotekeleza miradi yake kwa weledi.
Mama huyo mchapa kazi hakusita kuendelea kutoa yake ya moyoni kuhusu majengo yanayobuniwa na TBA kuwa ni ya kisasa na yanaishi kwa muda mrefu.
“Sisi kama nchi tunajivunia kuwa nanyi tunaona kabisa kuwa TBA iko tayari na uwezo wenu kwa sasa huenda si tu wa kufanya kazi ndani ya nchi huenda hata nje ya nchi mna uwezo wa kufanya” anasisitiza Mhe. Senyamule.
Katika mkoa wa Geita TBA inatekeleza miradi kadhaa ikiwemo ujenzi wa hospitali ya Rufaa ya Kanda, Chato, hospitali ya Rufaa ya Mkoa, Jengo la Ofisi ya mkuu wa mkoa, Tanesco, soko la mnada wa mifugo, nk.