Mpango wa Ununuzi unaoandaliwa utakuwa si tu chachu ya utekelezaji wa majukumu ya TBA kwa viwango, ubora na wakati unaostahili bali utaweka malengo na mwelekeo wa manunuzi ya Wakala kwa mwaka wa fedha 2023/24 na hivyo kufanya maboresho makubwa na kuondoa mapungufu yaliyojitokeza huko nyuma. Hayo yamesemwa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) Arch. Daud Kondoro wakati akifungua Kikao Kazi cha Uandaaji wa Mpango wa Ununuzi wa TBA kwa mwaka 2023/24 kinachofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa St. Gasper jijini Dodoma.
Pia Arch. Kondoro ameainisha kuwa Mpango wa Ununuzi ni kitendea kazi muhimu ambacho kitahakikisha kuwa utekelezaji wa shughuli za Ununuzi wa Kandarasi, Huduma na Vifaa kwa ajili ya TBA unakamilika kwa muda uliopangwa na kwa kuzingatia Sheria na Kanuni za Ununuzi wa Umma.
Arch. Kondoro amesema anamatarajio makubwa kuwa Timu itaandaa Mpango wa Ununuzi utakaotekelezeka hivyo kuwezesha kufikia malengo ya Wakala na Serikali kwa ujumla. “Ni kazi ya Timu sasa kuhakikisha kuwa Mpango wa Ununuzi utakaoandaliwa unaenda kutoa mchango wa kutosha katika kuufanya Wakala kufikia maono ili kuchangia kikamilifu Maendeleo ya Taifa” amesema Arch. Kondoro.
Awali akimkaribisha Mtendaji Mkuu, Meneja wa Kitengo cha Ununuzi na Ugavi Bibi Mariam Kazoba ameeleza kuwa kazi ya uandaaji wa mpango wa Ununuzi wa mwaka 2023/24 itafanyika kwa njia shirikishi ambapo kila Idara, Kitengo, Sehemu na Kanda itaainisha mahitaji yake na kubainisha kiasi cha fedha kitakachotumika kutekeleza ununuzi wa mahitaji hayo kwa kuzingatia mpango na bajeti ya TBA ya mwaka 2023/24 ili kuandaa Mpango wa Ununuzi ulio bora na utakaotekelezeka na hatimaye kufikia malengo yaliyowekwa.
PROCUREMENT PLAN SETTING GOALS AND PURCHASING DIRECTION - TBA CHIEF EXECUTIVE.