Watumishi wa Taasisi mbalimbali za Serikali mkoani Mbeya, wamevutiwa na Mradi wa nyumba za makazi – Bunju unaotekelezwa na Wakala wa Majengo Tanzania (TBA). Watumishi hao wameonyesha nia ya kuzinunua nyumba hizo baada ya uwasilishwaji uliofanywa na TBA katika Taasisi zao.
Wakizungumzia katika Mkutano wa uwasilishwaji wa Mradi huo
wamesema, nyumba hizo zimejengwa kwa kiwango ambacho kinakidhi mahitaji ya
watumishi wa umma hivyo wameshauri mradi huo pia ufanyike katika mikoa mingine
ya Tanzania ukiwemo mkoa wa Mbeya ili watumishi wengi wapate fursa ya kununua
nyumba hizo ambazo bora na Bei nafuu.
Katika Mkutano huo, aina tofauti za nyumba ziliwasilishwa, Bei na utaratibu wa kununua nyumba hizo. Miongoni mwa Taasisi zilizoshiriki uwasilishwaji huo ni Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF), Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA), Shirika la Bima la Taifa (NIC), Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA), Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Wakala wa Ufundi na Umeme Tanzania (TEMESA), Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) na Wakala wa Afya Mahala pa Kazi (OSHA).