Bodi ya Ushauri ya Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) imetembelea na kukagua maendeleo ya mradi wa ujenzi wa nyumba za makazi katika eneo la Temeke Kota jijini Dar es Salaam.
Akizungumza mara baada ya ziara hiyo Mwenyekiti wa Bodi hiyo Arch. Dkt. Ombeni Swai amesema ziara hiyo ni muendelezo wa ufuatiatiliaji wa miradi inayotekelezwa na TBA.
"Leo tumepata nafasi ya kutembelea mradi huu ikiwa ni muendelezo wa kukagua maendeleo ya miradi inayotekelezwa na TBA katika maeneo mbalimbali nchini. Ni imani yetu kuwa malengo ya mradi huu ni kutatua changamoto ya makazi kwa wakaazi mbalimbali wa jiji la Dar es salaam amesema Arch. Dkt. Swai.
Pia Arch. Dkt. Swai amesema wanatarajia kuwa utekelezaji wa mradi huo unazingatia vigezo vyote ikiwa ni pamoja na ubora na gharama za ujenzi.
Aidha, Arch. Dkt. Swai ameiomba Serikali kutoa fedha kwa wakati ili kufanikisha malengo ya utekelezaji wa mradi huo kwa wakati.
Akiongelea miaka miwili ya Mhe. Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan madarakani,
Arch. Dkt. Swai amesema TBA imefanikiwa kutekeleza miradi mingi ya ujenzi ikiwa ni pamoja na utekelezaji wa miradi ya ujenzi wa nyumba za Makazi kwa watumishi wa Umma katika maeneo ya Magomeni Kota, Canadian Masaki na eneo hili la Temeke Kota jijini Dar es Salaam.
Kwa upande wake Mtendaji Mkuu wa TBA Arch. Daud Kondoro amesema ziara hiyo ni muhimu kwa TBA kwakuwa inatoa fursa kupokea maoni na ushauri juu ya utekelezaji wa mradi huo ambao unatarajiwa kuchukua idadi kubwa ya Wakaazi.
Bodi ya Ushauri ya TBA imefanya ziara katika mradi wa ujenzi wa Nyumba za Makaazi katika eneo la Temeke Kota ambapo mradi huo unatekelezwa na TBA kama Mkandarasi na Mshauri Elekezi.