Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) umekabidhi jengo la Mahakama ya Wilaya ya Kwimba lililogharimu takribani shilingi bilioni 1.1. Mradi huo wa ujenzi wa jengo la Mahakama umesimamiwa na TBA huku Mkandarasi akiwa ni KIURE Engineering and Construction Company.
Akizungumza wakati wa makabidhiano hayo Mtendaji Mkuu wa Mahakama Kanda ya Ziwa Bw. Nestory Mujunangoma amesema "Sina shaka na utendaji wa TBA, wamekuwa wakijenga kwa ubora na weledi miradi mingi ya Mahakama ikiwemo usimamizi wa jengo la Kituo Jumuishi Kanda ya ziwa linalojengwa jijini Mwanza”.
Naye Mbunifu Majengo Suzanne Boniface akimuwakilisha Meneja wa TBA Mkoa wa Mwanza amesema jengo hilo limezingatia viwango vya ubora kwani wamekuwa wakimsimamia Mkandarasi hatua kwa hatua. Pia ameongeza kuwa TBA itaendelea kutekeleza miradi mingi kwa ubora na kwa wakati kulingana na mkataba.