Wakala wa Majengo Tanzania (TBA), umemkabidhi Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Vigaeni Bi. Salama Buhanga ofisi ambayo imefanyiwa ukarabati mkubwa kama sehemu ya kurudisha kwa jamii.
Akizungumza katika Hafla fupi ya kukabidhi ofisi hiyo,Kaimu Meneja wa TBA mkoa wa Dar es Salaam Arch. Bernad Mayemba kwa niaba ya Mtendaji Mkuu wa TBA Arch. Daud Kondoro ameishukuru serikali ya mtaa wa vigaeni kwa ushirikiano wanaoutoa katika kipindi chote ambacho TBA inaendelea kutekeleza miradi yake katika mtaa huo ambao umewawezesha kutekeleza majukumu yao kwa urahisi.
Akizungumzia ukarabati uliofanyika katika ofisi hiyo Arch. Mayemba amesema umejumuisha kupaka rangi, kuweka gymsum board, aluminium, grills, paving blocks, tiles, ukarabati kwenye paa pamoja na uwekaji wa feni na taa ambao umegharimu takribani milioni tisa (9).
Naye Bi. Salama ameushukuru uongozi wa TBA kwa ukarabati walioufanya ambao umesaidia kutatua changamoto iliyokuwa ikiwakabili ya kuvuja kwa ofisi wakati wa mvua ambao ulikuwa ukipelekea mazingira ya kazi kwa watendaji wa ofisi hiyo kutokuwa rafiki.
Aidha, akizungumza baada ya makabidhiano hayo mwakilishi wa Diwani wa Kata ya Ndugumbi Bw. Acleus Mshumbushi amesema TBA imeacha alama kwa viongozi na wakazi wa Vigaeni kwa kufanya ukarabati wa ofisi hiyo.
Katika kutekeleza majukumu yake TBA imeendelea kurudisha kwa jamii ambapo kwa Mkoa wa Dar es Salaam imeshafanya ukarabati waKituo cha Afya cha Magomeni pamoja na kujenga vyoo na kukarabati ofisi za Walimuwa Shule ya Sekondari Juhudi iliyopo Gongolamboto Wilaya ya Ilala.