WAKALA wa Majengo Tanzania (TBA,) Umetoa majina ya wakazi wa Kaya 61 wa nyumba za makazi Magomeni Kota ambao wakati wa zoezi la ugawaji wa nyumba hizo walikuwa na migogoro ya kifamilia hasa kwa nyumba moja kuwa na umiliki wa zaidi ya mtu mmoja hali iliyopelekea Serikali kuingilia kati na kutafuta Suluhu.
Akizungumza wakati wa kukabidhi majina hayo kwa uongozi wa makazi hayo Katibu Tawala wa Wilaya ya Kinondoni na mlezi wa makazi hayo Bi. Stella Msofe ambaye alimwakilisha Mkuu wa Wilaya amesema changamoto hiyo ya watu 61 ilisababishwa na wananchi wenyewe na katika kuhakikisha kila mwananchi anapata stahiki yake Serikali kwa kushirikiana kwa karibu na watekelezaji wa mradi huo TBA walifanya uchunguzi wa kina na kubaini wanaostahili kuingia katika nyumba hizo.
‘’Baada ya changamto zote Serikali imefanya uchunguzi wa kina wa kubaini nyaraka, kuhoji watu ana kwa ana na kuhoji watu wengine…timu imefanya kazi kwa haki katika kubaini nani anastahili kuingia katika nyumba hizi.’’ Amesema.
Pia amesema kuwa wakazi hao lazima wawe waangalizi wa miundombinu katika makazi hayo na hiyo ni pamoja na kuchanga gharama za huduma jumuishi kama walivyokubaliana.
”Wanakota tushiriki katika kutoa michango ya huduma jumuishi ili kuendelea kuweka miundombinu ya makazi haya vizuri zaidi nimeelezwa hapa kati ya wakazi 583 walioingia katika nyumba hizi wakazi 250 pekee wamechangia gharama za huduma hizo na shilingi milioni kumi laki mbili na elfu thelathini zimekusanywa tunafahamu Serikali imemaliza muda mlioomba na jukumu hilo litahamishiwa kwa viongozi wenu katika kusimamia gharama za huduma jumuishi kutoka kwenu na atakayekaidi Serikali ipo itamchukulia hatua.’’ Alisema.
Aidha amewaonya vijana ambao wamekuwa wakionesha vitendo visivyo vya kimaadilii ikiwemo kuwaingiza watu wasiohusika katika nyumba hizo na kuonesha taabia chafu ikwemo kuvuta bangi na kueleza kuwa Serikali ipo macho na yeyote atakayebainika atachukuliwa hatua kali.
Pia Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) Arch. Daud Kondoro amesisitiza kuwa zoezi la kukabidhi kwa nyumba hizo kwa wenye stahiki litafanyika ndani ya wiki moja pekee na hiyo ni baada ya Serikali kupata majibu baada ya uchunguzi na uchambuzi wa taarifa zilizokusanywa na timu maalum iliyoundwa kuchunguza migogoro ya umiliki kwa wakazi hao 61.
”Majina, namba za nyumba, aina ya mgogoro na mwenye stahiki yameorodheshwa katika taarifa ambayo inakabidhiwa kwa viongozi wenu leo na tumeandaa utaratibu wa kukabidhi nyumba hizo kwa wenye stahiki kwa muda wa wiki moja pekee kuanzia wiki ijayo.’’ Alisema.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Idara ya Miliki kutoka Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) Said Mndeme amesema kuwa nyumba za makazi katika eneo hilo zilijengwa kwa ajili ya wakazi 644 waliokuwa wakiishi katika eneo hilo na baada ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan kuzindua na kukabidhi nyumba hizo kwa walengwa wakazi 583 walipata fursa ya kuingia katika nyumba hizo na wakazi 61 walishindwa kuinga katika nyumba hizo kutokana na migogoro ya kifamilia.
Amesema asilimia 80 ya migogoro ilikuwa ya kifamilia hasa kwa wazazi waliofariki na wahusika kuwa zaidi ya mmoja katika umiliki na nyumba hizo, Serikali ilitumia busara kwa kuunda timu maalum ambayo iliwahoji wahusika pamoja na kutafuta taarifa zaidi ili wenye stahiki na nyumba hizo waweze kukabidhiwa.
Vilevile Mwenyekiti wa Mtaa wa Magomeni Kota George Abel ameishukuru Serikali kupitia TBA kwa kutumia hekima na busara ya kuingilia kati na kutatua migogoro hiyo kwa wakazi 61 wa eneo hilo.
Amesema, baada ya TBA kumaliza muda wa kusimamia gharama za huduma za jumuishi, wakazi wa makazi hayo wataanza kuchangia huduma hizo kuanzia Agosti Mosi mwaka huu na kuwataka kutotunisha misuli na badala yake kuiunga mkono Serikali ili kuendelea kuweka salama miundombinu ya makazi yao kwa muda mrefu.
Pia amemshukuru Mtendaji Mkuu wa TBA na timu nzima ya Wakala hiyo kwa kuendelea kuwasaidia katika utatuzi wa changamoto mbalimbali ikiwemo ya kutafuta suluhu ya migogoro kwa wakazi 61 wa Magomeni Kota.