Wakala wa Majengo
Tanzania (TBA), imenunua Mitambo ya kuchakata zege pamoja na Mashine za
kutengeneza tofali ambazo zitatumika kupunguza gharama za ujenzi katika miradi mbalimbali inayotekelezwa na TBA ukiwemo Mradi
wa nyumba za makazi Magomeni Kota.
Hayo yamesemwa na
Mhandisi Mkuu wa TBA, Jasper B. Lugemarila, aliyemwakilisha Kaimu Mtendaji Mkuu
wa TBA, wakati wa ziara ya Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
anayesimamia Sekta ya Ujenzi, Mhe. Elias
John Kwandikwa, alipofanya ziara ya kukagua Maendeleo ya Mradi wa Makazi
wa Magomeni Kota, Aprili 13, 2019
Katika ziara hiyo, ilielezwa
kuwa changamoto kubwa iliyosababisha kutokamilika kwa mradi huo kwa wakati ni
mfumuko wa bei za malighafi ambazo kwa sasa zimepatiwa ufumbuzi kwa baadhi
kuanza kuzalishwa na TBA wenyewe.
Mhandisi Lugemarila, alimhakikishia
Mhe. Naibu Waziri kuwa wameshaandaa mpango kazi ambao utafuatwa kikamilifu ili
waweze kukamilisha ujenzi huo kufikia mwishoni mwa mwaka huu.
Baada ya kukagua Maendeleo
ya Ujenzi huo, Naibu Waziri Kwandikwa, alisisitiza kutoa ushirikiano kwa TBA
ili waweze kukamilisha ujenzi wa Mradi huo kwa wakati kulingana na Mkakati huo
mpya uliyoandaliwa.
Ujenzi wa nyumba za
Magomeni Kota ukikamilika, utachangia kwa kiasi kikubwa kutatua changamoto ya
makazi kwa familia 656, zikijumuisha familia 544 zilizokuwa zikiishi katika
eneo hilo hapo awali.