Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) Imeendelea kuandika historia katika mkoa wa Geita kwa kutekeleza miradi mikubwa ya Ujenzi inayopeleka huduma kwa wananchi ambapo tarehe 11 Januari 2023 imekabiidhi Jengo la ofisi ya Tanesco mkoa wa Geita.
Akipokea funguo kuashiria kukabidhiwa Kwa jengo hilo, Meneja wa Tanesco mkoa wa Geita, Bi. Grace Mtungi alisema “Kwa kweli tumefurahi sana kupata jengo hili lenye viwango vya hali ya juu tena kwa wakati, lilikuwa tamanio letu la muda mrefu tuwe na jengo kubwa hivi kutokana na ufinyu wa jengo lililokuwa likitumika kabla, Lakini vilevile itatusaidia kupunguza gharama tulizokuwa tukizitumia kwa mwaka kiasi cha shilingi milioni ishirini na nne (24) kama pango kwa jengo la ofisi. Lakini sasa Maafisa wa Tanesco wataweza kuwahudumia wateja wetu katika hali nzuri ya usikivu ambao tunaamini hata wateja wetu waliutamani Kwa muda mrefu”. Vilevile Bi.Grace akatumia nafasi hiyo kumshukuru Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha nyingi katika kufanikisha mradi huo mkubwa na mingine mingi mikubwa ambayo itafanikisha upatikanaji wa umeme wa uhakika na kuchangia maendeleo ya mkoa wetu, lakini kwa namna ya kipekee niwashukuru Wakala wa Majengo kwa kutupa ushirikiano mkubwa hadi kufanikisha kukamilika kwa mradi wa Ujenzi wa Majengo yetu ya Tanesco hapa Mkoani Geita na kule Wilayani Chato.
Akizungumza Kwa niaba ya Wasimamizi na washauri wa mradi huo uliokabidhiwa Arch. Godfrey Mwakabole, amesema TBA ipo kuhakikisha inazingatia ubora na ujenzi wenye tija ambao unatufanya kuwa tofauti hasa linapokuja suala la kusimamia ubora lakini vilevile tunajitahidi kukamilisha miradi yetu ndani ya muda unaokuwa umepangwa.
Wakala wa Majengo Tanzania licha ya Ujenzi wa Ofisi za Tanesco katika mkoa Geita, lakini pia umeendelea kutekeleza miradi mbalimbali ya kimaendeleo katika sekta mbalimbali kama vile Utekelezaji wa mradi mkubwa wa Hospital ya Rufaa ya Kanda Chato.