TBA YAPONGEZWA KWA UTEKELEZAJI WA MIRADI YA MAENDELEO MKOANI TABORA
Wakala
wa Majengo Tanzania (TBA) wapongezwa kwa kuendelea kutekeleza miradi ya
maendeleo Mkoani Tabora. Uongozi wa Mkoa wa Tabora ulitoa jukumu kwa TBA
kusimamia na kujenga miradi ya maendeleo kwa ubora na viwango vinavyohitajika
katika majengo mbalimbali mkoani humo.
Hatua
ya kuipongeza TBA Mkoani Tabora imekuja baada ya Katibu Tawala Wilaya ya Kaliua
Bw. Michael Nyahinga kujiridhisha na hatua ya utekelezaji wa miradi ya ujenzi
wa nyumba za viongozi katika Wilaya ya Kaliua. Bw. Nyahinga alisema TBA
imefanya kazi kubwa na nzuri ambayo inastahili pongezi kwani nyumba hizo zina
ubora na zimejengwa kwa wakati ndani ya mkataba.
Kaimu
Meneja wa TBA Mkoa wa Tabora Mhandisi Abraham Ndazi amesema TBA inatekeleza
miradi ya aina tatu ambayo ni Ubunifu na Ujenzi, Ushauri pamoja na ukarabati. Miradi
ya Ubunifu na Ujenzi inayotekelezwa Mkoani Tabora ni pamoja na ujenzi wa Nyumba
ya makazi ya Katibu Tawala wa Tabora mjini, Nyumba ya makazi ya Mkuu wa Wilaya
na Katibu Tawala Wilaya ya Kaliua pamoja na Nyumba za makazi za Maafisa Waandamizi
Wilaya ya Kaliua. Pia katika miradi ya Ushauri inayotekelezwa ni pamoja na
Ujenzi wa jengo la ofisi ya Halmashauri ya Wilaya ya Nzega, Ukarabati wa jengo
la Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Tabora na Ujenzi wa jengo la Utumishi wa Umma
Mkoani Tabora.
Aidha,
Mhandisi Abraham Ndazi alisema mafanikio ya utekelezaji wa miradi hiyo ya
maendeleo Mkoani Tabora yanatokana na ushirikiano mzuri unaotolewa na washitiri
kwa TBA. Vile vile Mhandisi Ndazi ameongeza kuwa ofisi yake ina mkakati wa kukarabati
karakana kwa lengo la kuzalisha samani ambazo zitakuwa na ubora na kuongeza
mapato kwa TBA.
Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) ni taasisi
ya Serikali iliyoanzishwa mwaka 2002 kwa lengo la kusimamia miliki za Serikali.