TBA YASHIRIKI UJENZI WA KITUO CHA PAMOJA CHA FORODHA KASUMULU
Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) unashiriki kama
Mshauri Elekezi Msaidizi (Sub-Consultant) katika utekelezaji wa mradi wa Ujenzi
wa Kituo cha Pamoja cha Forodha mpakani mwa Tanzania na Malawi unaoendelea
katika eneo la Kasumulu, Mkoani Mbeya. Mradi huu unatarajiwa kuwa na faida
kubwa katika kukuza ushirikiano baina ya nchi hizi mbili pamoja na kuchochea
fursa za kibiashara kati ya Tanzania na Malawi. Mradi huu utakapokamilika
utarahisisha usafirishaji wa watu na mizigo kutoka pande zote mbili hivyo
kuchochea ukuaji wa biashara pamoja na uchumi kwa ujumla.
Akielezea juu utekelezaji wa mradi huu,
Arch. Daniel Mandari amesema utekelezaji wa mradi unaendelea vizuri kwa
kuzingatia viwango vya ubora unaotakiwa. Pia amesema mradi huu ni muhimu kwa wananchi
na taifa kwa ujumla kwa kuwa utakuza wigo wa bishara kati ya Tanzania na
Malawi.
Arch. Mandari aliongeza kuwa katika mradi huu,
TBA kama Mshauri Elekezi Msaidizi (Sub-Consultant) inashirikiana vizuri na kampuni
ya CGC kutoka China ambayo ndiyo mkandarasi na kampuni ya EGC kutoka Misri
ambayo ndiyo Mshauri Elekezi. Pia alieleza kuwa mradi huu unakabiliwa na
changamoto ya mvua ambayo kwa kiasi fulani inaathiri kasi ya utekelezaji wa
mradi kwa sababu kazi za ujenzi wa barabara zinaathirika sana na uwepo wa mvua
zinazoendelea kunyesha nchini.
Kwa upande wa Meneja mradi kutoka kampuni ya
CGC, Mhandisi Zhao amesema katika kutekeleza mradi huu huwa wanajadiliana na
wataalam wa TBA kwa kila hatua ya utekelezaji wa mradi na wakikubaliana
wanaendelea na kazi. Aliongeza kwa kusema kuwa wataalam wa TBA wana uzoefu
mkubwa na kunapokuwa na mashaka na kitu wanapata nafasi ya kuwauliza na kupokea
mapendekezo yanayowawezesha kufanya kazi nzuri na kwa viwango vinavyohitajika.
Imetolewa
na Kitengo cha Mawasiliano kwa Umma na Masoko – TBA
25
Machi, 2020