Wapangaji ambao ni watumishi wa umma, wameanza kuingia kwenye nyumba za Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) katika mradi wa ujenzi wa nyumba 3500 za makazi zilizopo eneo la Nzuguni Jijini Dodoma.
Mpaka sasa, jumla ya nyumba 150 kati ya 3500 tayari zimejengwa katika mradi huu ambao unatekelezwa kwa awamu hadi kukamilika kwake. Maafisa wa TBA, wameonekana wakitekeleza majukumu yao kwa ufanisi kuwapokea watumishi hao wanaoingia katika awamu hii ya kwanza.
Mmoja wa wapangaji hao, Bi. Susan Adam ambaye anafanya kazi Halmashauri ya Jiji la Dodoma, ameshukuru kupata nyumba TBA ambayo amesema, itasaidia kuondoa changamoto ya makazi aliyokuwa nayo siku za nyuma.
Naye Bw. Thomas Mwakimata, mfanyakazi kutoka ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), amepongeza TBA kwa ujenzi wa nyumba hizo ambazo amebainisha kuwa zimejengwa kwa ustadi na ubora mkubwa.
Bi. Liliani Kiugi ambaye anafanya kazi Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA) baada ya kukabidhiwa nyumba amesema " Nawashukuru sana TBA, nyumba hii ni kubwa na nzuri na mazingira yote yanayozunguka nyumba ni mazuri, hongereni sana TBA"
Afisa kutoka Idara ya Miliki TBA Bw. Emmanuel Pesambili ambaye anasimamia zoezi hili anabainisha kuwa, kabla mpangaji hajakabidhiwa funguo ya nyumba anapitishwa kukagua kuona kama mifumo yote ikiwemo maji, umeme, milango na madirisha inafanyakazi vizuri na ili kama kuna changamoto yoyote iweze kurekebishwa.
Mradi wa ujenzi wa nyumba 3500 za makazi Nzuguni unatekelezwa kwa lengo la kupangisha watumishi wa umma ili kuondoa changamoto ya makazi kwa watumishi hao mkoani Dodoma