Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji ya Mitaji ya Umma (PIC) imeitaka Serikali kuiwezesha TBA. Hayo yamesemwa na Mwenyekiti na Kamati hiyo Mhe. Deus Sangu (Mb) wakati wa ziara ya kutembelea na kukagua maendeleo ya utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa nyumba za makazi katika eneo la Magomeni Kota awamu ya pili jijini Dar es Salaam.
Akizungumza wakati wa ziara hiyo Mhe. Sangu amesema kuwa TBA imefanya uwekezaji wenye tija.
"Katika kikao chetu na Menejimenti ya TBA tumepata fursa ya kuoneshwa mpango wa ujenzi wa majengo ya makazi katika eneo hili la Magomeni Kota ambapo tumeshuhudia jengo moja limekamilika na jengo la pili likiwa limefikia 96%" amesema Mhe. Sangu.
Vile vile Mhe. Sangu amepongeza uwekezaji huo uliofanywa na TBA kuwa unakwenda kutatua changamoto ya makazi kwa wakaazi mbalimbali wa jiji la Dar es Salaam kwa kupata makazi ya uhakika.
Pia Mhe. Sangu ameitaka Serikali kuhakikisha inatoa fedha kwa wakati ili kukamilisha mpango huo wa ujenzi wa majengo matano katika eneo hilo la Magomeni Kota kwa lengo la kuharakisha upatikanaji wa makazi kama ilivyokusudiwa.
Aidha, Mhe. Sangu ameishukuru Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuruhusu kufanyika uwekezaji ambao unagusa wananchi wa hali zote.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri ya TBA Arch. Dkt. Ombeni Swai ameishukuru Kamati kwa kufanya ziara hiyo na kuahidi kuendelea kuisimamia Menejimenti ya TBA katika kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi.