Wafanyakazi wa Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) wamempongeza na kumshukuru Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kutimiza ombi la wafanyakazi la kuongeza mshahara na kutimiza ahadi aliyoitoa wakati wa sherehe za siku ya wafanyakazi zilizofanyika Kitaifa katika uwanja wa Jamhuri mkoani Dodoma kwa kuongeza mshahara kwa asilimia 23.3.
Katika sherehe hizo Rais Samia, aliahidi kuongeza mshahara kwa wafanyakazi na kuwataka kutimiza wajibu wao kwa kufanya kazi kwa bidii ili kutimiza malengo ya Taasisi zao.
Bi. Magreth Ndemasi ambaye ni Mkadiriaji Majenzi (QS) amesema anamshukuru sana Mhe. Rais Samia kwa kusikiliza na kujibu kiu yao ambayo waliisubiri kwa muda mrefu.
“Binafsi namshukuru sana Mama kwa kusikia kilio chetu na ongezeko hili limetusaidia sana kutokana na hali ya maisha kwa sasa kupanda, bei ya bidhaa imepanda, hivyo nyongeza hii itasaidia sana kupunguza changamoto kadhaa. Niwaombe sana wafanyabiashara wasitumie kigezo hiki kupandisha kiholela bei za bidhaa”, alisema Magreth.
Naye Bi. Inocensia Ngonde ambaye pia ni Mkadiriaji Majenzi (QS) ameshukuru na kubainisha kwamba ni jambo ambalo wafanyakazi walilisubiri kwa muda mrefu.
“Sisi kama wafanyakazi wa Umma tunamuahidi Mhe.Rais tutafanya kazi kwa bidii na weledi mkubwa ili nchi yetu iendelee kupata tija na kuinuka kiuchumi”, amebainisha Bi. Inocensia.
Kwa upande wake Mhandisi Athanas Mussa amefafanua kwamba kwa kipindi cha miaka 5 hadi 6 hakukuwa na ongezeko lolote la mshahara, hivyo Rais Samia amesikia kilio cha wafanyakazi na kutekeleza ahadi yake.
Ongezeko la mshahara ni motisha kwa wafanyakazi wa Umma ambao wameahidi kuongeza juhudi katika utendaji wao wa kazi. Nao, wamewataka wafanyabiashara wasitumie fursa hii kama kigezo cha kupandisha bei za bidhaa.