Leo Novemba 18, 2022 Wakaguzi wa ndani wa Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi (Sekta ya ujenzi) wamefanya ziara ya kutembelea na kukagua miradi inayotekelezwa na TBA mkoani Dar es Salaam. Miradi iliyotembelewa inajumuisha mradi wa ujenzi wa nyumba za makazi katika eneo la Temeke, mradi wa ujenzi wa nyumba za watumishi wa umma katika eneo la Magomeni Kota, mradi wa ukarabati wa nyumba uliopo katika eneo la Ukonga.
Ziara hiyo ilikuwa na lengo na kuangalia hatua iliyofikiwa katika utekelezaji wa miradi hiyo pamoja na kutoa ushauri juu ya utekelezaji wa miradi hiyo kwa lengo kuongeza ufanisi.
Akizungumza wakati wa ziara hiyo Mkaguzi wa ndani (ujenzi) Bw. Melkior Fabian amesema ziara hiyo ina manufaa kwa kuwa inajiridhisha na hatua zilizofikiwa katika miradi.
"Kupitia ziara kama hizi tunapata fursa ya kupima kiwango cha utekelezaji wa miradi pamoja na kujua thamani ya pesa iliyotumika. Lakini nipende kusema kuwa TBA imefanya kazi kubwa kuanzia mradi wa Temeke Kota, ujenzi wa nyumba za Watumishi za Magomeni pamoja na mradi wa Ukarabati wa nyumba tulizoziona pale Ukonga" amesema Bw. Fabian.
Vile vile Bw. Fabian amesema maendeleo ya ujenzi wa miradi hiyo inaridhisha kwa kuwa ipo katika hatua mbalimbali.
"Tunafarijika kuona miradi yote tuliyotembelea ujenzi wake unandelea kwa kasi na kufuata taratibu zote" amesema Bw. Fabian.
Kwa upande wake Kaimu Meneja wa Mkoa wa Dar es Salaam Arch. Bernard Mayemba ameshukuru ujio wa wakaguzi hao kutembelea miradi hiyo.
"Tunapotembelewa na wakaguzi katika miradi yetu inatupa fursa ya kujitathimini na kujua ujenzi tunaoufanya unatazamwa vipi. Lakini kwa sasa mradi wa ujenzi wa Temeke Kota umefikia asilimia 5 na kazi mbalimbali zinaendelea. Vile vile mradi wa ujenzi wa nyumba za watumishi wa Umma katika eneo la Magomeni Kota umefikia asilimia 91 ambapo matarajio yetu kufikia Desemba mwaka huu tuwe tumekamilisha" amesema Mayemba.