Wanafunzi kutoka Chuo Kikuu cha Lund nchini Sweden na wanafunzi kutoka Chuo Kikuu cha Ardhi cha hapa nchini wamefanya ziara ya kutembela mradi wa ujenzi wa nyumba 644 za makazi za Magomeni Kota, Kinondoni Jijini Dar es Salaam ambao tayari umeshakamilika.
Ziara hiyo ambayo ilikuwa na lengo la kujifunza masuala mbalimbali yanayohusu fani ya usanifu na ujenzi wa Majengo ambapo Katika ziara hiyo wanafunzi hao waliambatana na walimu wao na kupokelewa na Msimamizi wa Nyumba 644 Arch. Bernard Mayemba.
Akizungumza juu ujenzi wa nyumba hizo Arch. Mayemba amesema ujenzi wa nyumba hizo ni wa kisasa na umezingatia mahitaji husika.
“ Mradi huu umezingatia mahitaji husika kwa kuwa eneo yalipojengwa majengo haya yamechukua ekari tisa (9) katia ya ekari 32 ambazo nyumba ndogo ndogo wakati huo zilikuwa zimejengwa. Vile vile tumezingatia huduma mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuhakikisha kuwa tunaweka huduma muhimu ikiwa ni pamoja na umeme, maji na usalama wa mali na wakaazi” amesema Mayemba.
Vile vile Arch. Mayemba amezungumzia namna TBA ilivyo hakikisha kuwa inaendeleza eneo lililobaki kwa kufanya uwekezaji wenye tija.
“ Napenda kuwajulisha kuwa kuna soko ambalo linahudumia hao wakazi pamoja na wananchi wengine wa maeneo haya lengo likiwa ni kupunguza changamoto ya upatikanaji wa huduma za msingi ikiwa ni pamoja na chakula na mambo mengine. Pia tunaendelea na ujenzi wa soko la kisasa yaani Shopping Mall pamoja na ujenzi wa ghorofa saba (7) kwa ajili ya watumishi Umma lengo likiwa ni kutatua changamoto ya makazi” amesema Mayemba.
Aidha, Mayemba hakusita kutoa shukrani za dhati kwa niaba ya Mtendaji Mkuu kwa ugeni huo kuamua kuja TBA kujifunza mambo mbalimbali hasa kupitia mradi wa ujenzi wa nyumba 644 za makazi za Magomeni Kota.
Arch. Laura Liuka ambaye ni Mwalimu wa wanafunzi hao amesema amestaajabishwa na ubunifu na ujenzi uliofanywa na TBA kwa kuwa umezingatia mahitaji ya wakaazi na kutumia eneo dogo kwa kuchukua kiwango kikubwa cha wakaazi. Pia amesema kupitia ziara hiyo anaamini kuwa wanafunzi watakuwa wamejifunza mbinu mbalimbali za ubunifu wa nyumba za makazi ambazo watazitumia pindi watakapopewa nafasi.
Nyumba hizi 644 za makazi ambazo zimebuniwa na kujengwa na TBA, zimeendelea kuwa kivutio kwa wadau na wataalam wa masuala ya ujenzi ndani na nje ya nchi.