Waziri wa Nchi ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. Jenista Mhagama ameupongeza Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) kwa ubunifu mzuri wa majengo baada ya kutembelea na kukagua Jengo la Makao makuu ya Tume ya Maadili ya Utumishi wa Umma linalojengwa na TBA jijini Dodoma
“Nimeshuhudia ubunifu wa jengo zuri na lenye kuvutia, nina uhakika jengo hili likikamilika litakuwa bora na lenye kupendezesha mazingira ya eneo hili.” Ameeleza Waziri Jenista.
Sambamba na jengo hilo pia TBA imebuni majengo ya wizara mbalimbali yanayojengwa katika mji wa Serikali Mtumba, likiwemo jengo la Wizara ya Utumishi ambalo pia imebuni na inajenga yenyewe.
Awali akitoa taarifa za ujenzi huo kwa Waziri Mhagama, Meneja Sehemu ya Ujenzi TBA, Mhandisi Alinanuswe Mwakiluma amebainisha kuwa Mradi huo umetoa fursa kwa vijana wa Kitanzania kutoka vyuoni kuja kujifunza kwa vitendo na pia umezalisha ajira nyingi kwa watanzania hususani wakazi wa Dodoma ambao ni mafundi, vibarua, Baba na Mama lishe, machinga, waendesha bodaboda na kuwezesha kuongeza la pato lao.
Aidha, Mhe. Jenista Mhagama ameipongeza TBA kwa ubora wa mradi huo sambamba na ile inayoendelea katika mji wa Serikali Mtumba huku akibainisha kwamba miradi hii imechangia kwa kiasi kikubwa kuibuka kwa viwanda vingi vya Kitanzania vinavyozalisha marighafi za ujenzi.
“Nina uhakika miradi hii ikikamilika tutakuwa na wataalamu wengi pia viwanda navyo vitaongezeka” Amesisitiza Waziri Jenista.